Somo La 8 | Damu Isiyo Na Hatia

:
Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu


(Ayubu 10 & 15, Mithali 3)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Tunaona mfululizo wa tuhuma zinazotolewa na marafiki wa Ayubu pamoja na majibu yake kwao. Marafiki wanasema kuwa Ayubu anateseka kwa sababu ya dhambi zake. Ayubu anakana kwa kuwaambia kuwa hana hatia, na anampa Mungu changamoto kuthibitisha uhalali wa mambo yanayomtokea. Hii inawakasirisha marafiki wa Ayubu, kwa sababu wanakichukulia kitendo hiki kama shambulizi kwa Mungu. Je, hili ni shambulizi kwa Mungu? Je, jibu la kibinadamu juu ya mateso halina mwelekeo sahihi kwa sababu linamtaka Mungu kuhalalisha mateso? Je, jibu la kibinadamu juu ya mateso pia limejikita zaidi kwetu, badala ya kujikita kwa Mungu? Hebu tuchimbue somo letu la Ayubu ili tuone kile tunachoweza kujifunza!

I.                   Malalamiko ya Ayubu

A.                Soma Ayubu 10:1. Ayubu anasema kuwa anayachukia maisha yake. Kwa nini mtazamo huo unamfanya amlalamikie Mungu? (Ayubu anatafakari kuwa, “Ni jambo gani baya ambalo Mungu anaweza kunitendea, je, ni kuniua? Kwa kuwa Ayubu angependa kufa haoni kizuizi cha kutomlalamikia Mungu.)

1.                  Je, Ayubu ana sababu za msingi kimantiki? Je, unakubaliana na mantiki yake? (Ikiwa dunia ilikuwa inamzunguka Ayubu, basi jambo hili lingekuwa na mantiki. Lakini, ikiwa dunia inamzunguka Mungu, basi kuidhuru hadhi ya Mungu hakuna mantiki yoyote.)

B.                 Soma Ayubu 10:2-3. Ayubu anasema jambo moja kwenye fungu la pili, na anasema jambo jingine kwenye fungu la tatu. Unaweza kuyawekaje mambo haya mawili ayasemayo Ayubu kwa kutumia maneno yako mwenyewe? (Kwanza Ayubu anasema kuwa anataka kujua mashtaka dhidi yake ili aweze kujitetea. Lakini, katika fungu la tatu, Ayubu anasema jambo tofauti kabisa. Hatarajii haki kutoka kwa Mungu kwa kuwa Mungu anatafuta namna ya kumdhuru na wakati huo huo kuwabariki wale wanaotenda uovu.)

1.                  Je, unadhani kwamba kweli Ayubu anaamini kuwa Mungu anataka kumdhuru na wakati huo huo kuwapa thawabu watu waovu? (Napata ugumu kuamini hivyo. Nadhani Ayubu anasema maneno ya kufedhehesha na ya kikatili kama haya ili kujaribu kumchochea Mungu amjibu.)

2.                  Unaweza kuona hitilafu gani kwenye fikra ya Ayubu? (Ayubu anachukulia kwamba mambo yote haya yanamhusu. Hicho ndicho kinachofanya jambo hili lionekane kutokuwa la haki. Ayubu ni mwema, watu waovu ni wabaya, na hivyo Mungu ameshindwa kutenda haki. Hata hivyo, tunajua kwamba hali inayomkabili Ayubu haihusiani na suala la haki kwa ajili yake. Badala yake, mambo yanayomkabili Ayubu yanahusiana na pambano kuu kati ya wema na uovu.)


3.                  Je, Mungu anaweza kuhalalisha mambo yanayomtokea Ayubu? (Soma Ayubu 2:3. Mungu anakubali kwamba yaliyomtokea Ayubu si haki kwake.)

4.                  Tafakari jambo hili kidogo. Tunapoona vitendo visivyo vya haki vikitokea duniani, Mungu pia anaweza kukubaliana kwamba sio vitendo vya haki! Je, ni sahihi basi kumlaumu Mungu kwa vitendo hivyo visivyo vya haki?

C.                 Soma Ayubu 10:4-7. Unadhani jibu kwa maswali ya Ayubu ni lipi? (Jibu ni “hapana.” Mungu si kama mwanadamu, na Mungu hafuatilii kila dhambi ya Ayubu ili kumwadhibu.)

1.                  Kuna kasoro gani kwenye hii taswira ya Mungu? (Juma lililopita tulijifunza habari za Kora na waasi wenzake (Hesabu 16). Kwa dhahiri, Mungu anaweza (na amefanya hivyo) kutoa adhabu kwa ajili ya dhambi. Lakini, nadhani Mungu anatupatia sheria ili kutulinda dhidi ya dhambi. Mungu hataki tuteseke, hivyo anaweka bayana sheria yake ili tuweze kuyaepuka mateso. Hii ni taswira tofauti kabisa na ile iliyopendekezwa na Ayubu.)

D.                Soma Ayubu 10:12-14. Je, Ayubu anapotosha tabia ya Mungu? (Ndiyo! Tunajua ukweli ni tofauti na inavyoashiriwa na Ayubu hapa.)

1.                  Je, kuna wakati unakuwa na hatia ya kufikiria kama afikiriavyo Ayubu? Yaani, unaamini kwamba Mungu ni Mungu wa upendo, lakini anajificha kwenye tabia yake, shaukua yake ikiwa ni kukudhuru ikiwa hutamtii?

E.                 Soma Ayubu 10:15. Je, Ayubu “hana hatia?” (Ayubu ana dhambi, lakini tunajua kwamba haadhibiwi kwa kuwa mdhambi. Si hivyo hata kidogo! Anateseka kwa sababu yeye ni mwema sana (Ayubu 1:8-12). Kwa mara nyingine, Ayubu anatoka nje ya msitari kwa sababu anadhani kuwa dunia inamzunguka. Hafikirii kwamba mateso yake yanahusiana na utukufu wa Mungu.)

II.                Jibu la Elifazi

A.                Soma Ayubu 15:4. Rafikiye Ayubu, Elifazi, analeta shtaka jipya dhidi ya Ayubu. Anasema kwamba Ayubu anahafifisha uchaji Mungu na kuzuia ibada kwa Mungu. Unauchukuliaje ukweli wa shtaka hili? (Nadhani Elifazi yuko sahihi kwa mtazamo wa kibinadamu. Ayubu anapoleta mashtaka kwamba Mungu hatendi haki, hiyo inahafifisha imani kwa Mungu. Katika taswira ya kimbingu, kinyume cha jambo hilo ndio ukweli halisi.)

B.                 Soma Ayubu 15:7-9. Elifazi anatoa mashtaka kwa Ayubu kushindwa kuzielewa njia za Mungu. Je, Elifazi anadhani kuwa nani analemwelewa Mungu? (Elifazi anadhani kuwa yeye ndiye anayemwelewa.)

1.                  Je, Elifazi yuko sahihi kwamba Ayubu hamwelewi Mungu? (Ndiyo. Ayubu haelewi kile anachokifanya Mungu. Endapo Ayubu angekuwa sehemu ya baraza ambapo Shetani alimpa Mungu changamoto, Ayubu angeelewa mambo yanayoendelea.)


2.                  Je, Elifazi anamwelewa Mungu? (Hapana. Hii ni kejeli kubwa hapa. Elifazi yuko sahihi kwamba Ayubu haelewi kile ambacho Mungu anakifanya juu yake. Lakini, Elifazi pia hafahamu. Wote wawili hawaelewi kile ambacho kimsingi kinaendelea mawazoni mwa Mungu.)

3.                  Kuna kosa gani ambalo ambalo Ayubu na Elifazi wanalifanya kwa pamoja? (Wote wanafikiri kwamba sakata hili “linamhusu Ayubu.” Elifazi anadhani kuwa Ayubu anateseka kwa sababu alitenda dhambi. Ayubu anamshtaki Mungu kwa kutomtendea haki kwa sababu anajua kwamba hastahili yote haya. Wote wawili wanakosea kudhani kuwa mtu wa kuhusianishwa ni Ayubu.)

4.                  Chukulia kwamba mambo ya kutisha yanakutokea, kama yalivyomtokea Ayubu. Utasema nini ikiwa nitakuambia (kama ambavyo nimekuwa nikipendekeza hapa) kwamba mateso yako hayakuhusu? (Nahisi utakuwa tu kama Ayubu. Kimsingi mateso yako yanakuhusu wewe, ni suala binafsi kabisa!)

III.             Changamoto ya Imani

A.                Soma Mithali 3:5-6. Unaweza kuwatathminije Ayubu na marafikize kwa mujibu wa maelekezo haya? (Wote walikuwa wabaya kwa mujibu wa “usizitegemee akili zako mwenyewe!” Ama walisema mambo ambayo ni kweli kiteolojia, kimantiki, au ya kweli kwa mujibu wa uzoefu na uelewa wao wa mambo ya hapa duniani. Wote walikubaliana kwamba watu waliomtii Mungu walisitawi na wale ambao hawakumtii Mungu walipata mateso. Ayubu, huku akiamini (kwa usahihi) kwamba hakustahili mambo yote haya, alimshtaki Mungu kwa kutotenda haki. Yote haya yalikuwa na mantiki sahihi kabisa.)

1.                  Isipokuwa kwa jambo moja. Fungu hili linasema kuwa tufanye nini kwa uelewa wetu (sahihi) wa jinsi dunia inavyoenenda? (Tunatakiwa tuwe na imani kwa Mungu kwa kiwango cha juu zaidi hata ya uelewa sahihi wa teolojia, mantiki na uzoefu.)

2.                  Sasa hivi katika dunia hii kuna mambo ambayo yananitia hamasa sana, na mambo mengi ambayo hayanifurahishi kabisa. Watu wasio na uelewa wa Biblia (mbumbumbu wa Biblia), watu ambao ama ni wapumbavu kwa makusudi au walizaliwa hivyo, wanaiongoza dunia yangu. Je, ninapaswa kuwa na mwitikio gani kwa jambo hilo? (Kwanza, kumtumaini Mungu hata kama dunia haina mantiki yoyote. Pili, tunapokuwa hatujui cha kufanya, kwanza tunatakiwa “kumkiri” Mungu, naye atatuongoza.)

a.                   Unafikiriaje kumwomba Mungu aziongoze kazi (ayaongoze mambo yetu) zetu kivitendo? (Hapa ndipo mwongozo wa Roho Mtakatifu ulivyo wa muhimu sana. Tunatakiwa kuomba kupata uzoefu wa Yoeli 2:28-29, ambapo uwezo wa Mungu unanena kupitia kwetu sote – bila kujali utajiri wetu, jinsi yetu, umri wetu au uzoefu wetu.)

B.                 Soma Mithali 3:7-8. Ikiwa tunamcha Mungu na kujiepusha na uovu, je, mambo yetu yote yatakwenda barabara? (Hii inaturejesha tena katika mustakabali wa Ayubu. Soma Ayubu 1:8. Hivi ndivyo haswaa ambavyo Mungu anamuelezea Ayubu! Tunaweza kuiamini Biblia, lakini kama hakuna jambo linaloleta mantiki kwetu sasa kama wanadamu, basi tunatakiwa tu kumtumaini Mungu.)


C.                 Soma Mathayo 27:45-46. Je, Yesu amepitia uzoefu huu – kwamba sasa mambo yote hayana mantiki kwake? (Hivyo ndivyo kwa usahihi kabisa Yesu anavyoonekana kudhani.)

D.                Rafiki, je, utajitoa na kudhamiria kumtumaini Mungu leo, hata kama mawazo yako yanakuambia kuwa mambo yote hayako sahihi? Hata pale unapodhani kuwa Mungu amekuacha?


IV.             Juma lijalo: Udhahiri wa Matumaini.

No comments:

Post a Comment