Na Conges Mramba,Mwanza
Hospitali ya Wasabato Pasiansi mbioni kukamilika HOSPITALI ya wa-Adventista wa Sabato, iitwayo Mwanza Adventist Medical Centre(MAMC) ikikamilika kujengwa itakuwa imegharimu takriban shilingi bilioni tatu.
Mkurugenzi wa Afya na Kiasi wa Jimbo la Nyanza Kusini(SNC)Dk.Baraka Musa Maginga, alisema siku zilizopita kwamba kama washiriki wangetoa michango na sadaka zao kwa uaminifu, Hospitali hiyo iliyoko Pasiansi jijini Mwanza, ingeanza huduma katikati ya Julai mwaka huu 2016,kwa kuwa tayari vifaa vingi vipo.
Akizungumza nami katika Kanisa la Kirumba,jijini Mwanza,Dk. Maginga aliyekuwa akihimiza washiriki kutoa sadaka ya ujenzi wa Hospitali hiyo amesema MAMC itaanza kuhudumia wagonjwa kwa kutumia eneo la chini(Ground Floor) la jengo hilo na gorofa ya kwanza.
Amesema, hadi sasa kazi inayoendelea kufanywa ni pamoja na uwekaji wa madirisha,kupanga rangi na kuweka kingo za nje.
Aidha,Daktari huyo amesema serikali ilikuwa imewaruhusu Hospitali hiyo kuanza katika vyumba vya chini vya jingo hilo jipya,kwa kuwa hata sasa kuna huduma zinazoendelea kufanywa na kituo cha Afya.
Akizungumzia vifaa tiba, matabibu na madaktari,amesema vifaa vipo tayari na madaktari wapo wa kutosha kuanza kutoa huduma ifikapo Julai mwaka huu ambako amesema vyumba vitakavyokuwa tayari katika jengo hilo jipya vitaweza kuwekwa vifaa tiba kama mashine ya mionzi(X-ray),chumba cha upasuaji na Ultra Sound.
Hadi sasa Hospitali hii ya MAMC imetumia shilingi bilioni 1.9 ambazo ni michango na sadaka za wauamini; na itakapokamilika baadaye inatarajiwa kugharimu kiasi cha shilingi bilioni tatu.
Hospitali hii itaanza na jumla ya vitanda 100 vya kulaza wagonjwa hususan akina mama wajawazito watakaofika hospitalini hapo kujifungua.
Dk.Maginga amesema hospitali hiyo itafunguliwa baadaye mwaka huu na baadaye itakuwa na vyuo vya tiba,maabara na wafamasia.
Baadaye,MAMC inatazamiwa kuwa na jumla ya vitanda 450 vya kilaza wagonjwa,wakati zaidi ya wagonjwa 200 wa Nje(OPD) wakitibiwa kila siku na kuondoka.
Hadi sasa jiji la Mwanza lina Hospitali tatu za rufaa, hivyo MAMC itakapoanza rasmi kufanya kazi itakuwa inapunguza mrundikano wa wagonjwa katika Hospitali ya Bugando ambayo ina jumla ya vitanda 950 vya kulaza wagonjwa.
Hospitali nyingine zilizoko Mwanza ni Sekou Toure,Mwananchi na Nyamagana iliyoko Butimba wilayani Nyamagana.
Hospitali ya Bugando inayomilikiwa na Kanisa Katoliki ilianza mwaka 1972, na ni miongoni mwa Hospitali nne tu za Rufaa katika eneo la Magharibi mwa Tanzania na ukanda wa Ziwa Victoria ambako kuna takriban wakazi milioni 16 kati ya Watanzania milioni 45.
No comments:
Post a Comment