TUSIACHE KUMWOMBA MUNGU: SOMO LA WATOTO

Anita alikuwa ni mtoto mzuri sana. Aliishi magharibi wa Tanzania katika mkoa wa Kigoma. Siku moja Mama wa Anita alimuomba Anita waende porini kutafuta kuni. Basi wakaanza safari huku mama akiwa amembeba mdogo wa Anita mgongoni. Walipofika msituni mama alimwomba Anita amsubiri mahali fulani wakati yeye akitafuta kuni. Wakati mama akiwa anatafuta kuni, alisikia Anita akilia kwa sauti akisema “Mama Wananiiba?” Mama akakimbia mbio kwenda kumsaidia Anita. Kumbe watu wabaya walimbeba Anita na kukimbia naye. Mama aliomba msaada kwa wanakijiji lakini ilishindikana. 
Wakati huo Anita alikuwa analia sana huku akiwa amebebwa na watu wale wabaya. Wakati hayo yakiendelea, Anita akakumbuka jambo fulani. Akakumbuka kumuomba Mungu wake Akaomba akasema "Mungu unisaidie watu hawa wasinidhuru na ili siku moja niweze kuonana tena na wazazi wangu. Amina.” 
Basi watu wale wabaya, walipofika mbali, wakamwambia Anita, “Sisi hatuna nia mbaya na wewe. Wewe kazi yako itakuwa ni kuchunga mifugo yetu na hutalala ndani na sisi, na wala hutakula chakula pamoja na sisi.” Basi hayo ndio yakawa maisha ya Anita. Lakini watu wale walishangaa jambo moja kuhusu Anita. Tena kule kule kwenye mabanda ya mbuzi na kondoo, Anita alikuwa akiimba nyimbo za kumsifu Mungu. Wakashangaa maisha hayo. Basi, siku moja baba wa ile nyumba akamuuliza Anita, kwanini unainamba kila wakati? Anita akawaambia "Mimi namuimbia Mungu wangu aliye hai". Baba wa nyumba ile akamkemea Anita na kumkataza asiimbe wala kuomba kwa Mungu huyo. Na akamwamurisha awe anaandamana nao wanapokwenda kumwomba Mungu wao. Lakini Anita alikataa.
Basi, siku moja anita alikwenda kuchunga mifugo na alipokuwa anarudisha mifugo nyumbani wakati wa mchana, aliona watu wawili waliovalia mavazi meupe. Akawaza moyoni, huenda ni baba yangu, akasita na akajizuia kwenda kuwasalimia. Anita akaenda kujificha kwenye zizi. Akasikia watu wale wakisemezana wao kwa wao "Kesho twende kanisani. Kanisa halipo mbali na hapa. Lipo karibu na shule.” Anita akasikia maneno yale na kufurahi moyoni. Wale watu wakaondoka na Anita akaendelea na shughuli zake za kuchunga mifugo. 
Anita akaazimia kwenda kulitafuta lile kanisa ili awe aende huko kusali. Usiku ule Anita hakulala, alitamani asubuhi ifike aende kanisani. Basi asubuhi yake akawahi mapema na kuanza kunyata ili asionekane mwisho huyo akatimua mbio! Alikimbia kwa bidii na kila alipochoka alitafuta kichaka na kupumzika. Mara ya mwisho alipopumzika alishikwa na usingizi na kulala. 
Kule nyumbani kwa wale watu wabaya walipoamka walishangaa kuona mifugo inalia hovyo, wakagundua Anita hayupo na wakaanza kumtafuta. Lakini Anita alikuwa amekwenda mbali sana. hawakuweza kumpata.
Basi, Anita alipokuwa anazinduka kutoka pale kichakani alipolala, akasikia watoto wawili wanasemazana na mwisho wakamsogelea na kumuuliza kama anahitaji msaada. Anita akawaomba wampeleke kanisani. Wakamjibu wakamwambia hilo kanisa analoliulizia wanalijua maana walikuwa kwenye kanisa hilo juma lililopita. Basi wakampeleka Anita kanisani na akapokelewa na mchungaji. Mchungaji akaahidi kumtuza Anita na kumsaidia kuwatafuta wazazi wake. Mchungaji akasambaza matangazo kila mahali kwamba ana mtoto anayetafuta wazazi wake. 
Basi siku moja, wazazi wa Anita walipata taarifa za mtoto anayetafuta wazazi wakatembelea kanisa lile. Walipofika wakamuuliza mchungaji kwamba wangependa kumuona mtoto anayetafuta wazazi maana wao pia walipoteza mtoto ingawa hawana hakika kama aliuawa ama yupo hai. Mchungaji alipomleta mtoto kumbe alikuwa ni mtoto wao Anita. Walikumbatiana na kulia sana. Wazazi walimshukuru mchungaji kwa kumtunzia mtoto wao. Na kwa pamoja wakamshukuru Mungu kwa kulinda uhai wa Anita. 
Fundisho ni kuwa maombi ya Anita yalijibiwa, basi, tusiache kuomba, “Kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. (Luka 1:37” 

No comments:

Post a Comment