Somo la 6 | Kukufuru Bila Sababu?

Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu


(Ayubu 4)

Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.

Utangulizi: Marafiki wa Ayubu walikwenda kumtembelea na walishtuka kumwona akiwa katika hali ya kutisha (Ayubu 2:12). Je, umewahi kupitia uzoefu huo ulipomtembelea rafiki wako aliye mgonjwa? Ni vigumu kujua nini cha kusema. Kwa dhahiri, “kujisikia vibaya sana” halitakuwa jambo jema. Kama tulivyojadili hapo awali, marafiki wa Ayubu hawakusema neno lolote (Ayubu 2:13). Lakini, hawakuweza kustahimili jambo hilo kwa muda mrefu na wakaanza kujaribu kuyaelezea mateso ya Ayubu. Hapo ndipo tatizo lilipoanza. Hebu tuzame kwenye somo letu la Biblia ili tujifunze zaidi!

I.                   Lazima Utakuwa na Hatia ya Jambo Fulani

A.                Soma Ayubu 4:1-2. Je, Elifazi alidhamiria kuzungumza? (Ndiyo! “Ni nani awezaje kujizuia asiseme?” Mtu huyu ameshindwa kukaa kimya.)

B.                 Soma Ayubu 4:3-4. Unapokuwa unawakosoa watu, je, unaanza kwa kusema maneno mazuri juu yao ili “kupunguza ukali wa [mapigo]?”

1.                  Je, Elifazi anaanza kwa kusifia? (Ndiyo. Anasema kuwa Ayubu amekuwa akitoa ushauri mzuri mara nyingi wakati alipokuwa na hali nzuri kiafya.)

C.                 Soma Ayubu 4:5. Kwa kuwa Ayubu ni mshauri mwenye uzoefu, je, anapaswa kukabiliana na mateso vizuri zaidi?

1.                  Unaweza kufikiria sababu ambayo inaweza isiwe ya kweli? (Ni jambo moja kujadili mateso ya mtu mwingine, na ni jambo jingine kabisa kupitia mateso hayo wewe mwenyewe.)

D.                Soma Ayubu 4:6. Je, ushauri huu unasaidia au hausaidii? (Elifazi na Ayubu wana mtazamo fulani juu ya mateso – watu wabaya wanateseka na watu wema hawateseki.)

1.                  Ushauri huu unasaidia kwa namna gani? (Matatizo ya Ayubu yanapaswa kukoma kwa sababu yeye ni mtu mwema.)

2.                  Ni kwa jinsi gani ushauri huu hausaidii? (Ikiwa Ayubu anaendelea kuteseka, ni kwa sababu anayastahili mateso hayo.)

E.                 Soma Zaburi 119:65-67. Je, mtunzi wa Zaburi pia ana mtazamo sawa na Ayubu na Elifazi juu ya mateso? (Ndiyo. Ikiwa unadhani kuwa mateso yanasaidia kuboresha tabia yako, basi unakubaliana kwamba mateso yanatokana na tabia mbaya.)

F.                  Soma Ayubu 4:7-8. Endapo ungekuwa Ayubu, je, ungekuwa unafikiria nini wakati kama huu? (Elifazi hasemi hivyo kwa kuwa mimi ni mtu mwema, mateso yatakoma haraka, badala yake, anapendekeza kwamba tabia yangu mbaya ndio inayosababisha mateso yangu.)


G.                Hebu tutafakari jambo hili kidogo. Je, mtunzi wa Zaburi, Ayubu, na Elifazi hawako sahihi katika hili suala? Je, wamechanganya mambo kabisa? (Hapana. Wanaelewa mambo yaliyo ya dhahiri kwa wanafunzi wote makini wa Biblia. Ulimwengu wa Mungu unatawaliwa na kanuni. Kuna kanuni za asili (kama vile nguvu za mvutano) na kuna kanuni za mwenendo [tabia] (kama vile sheria dhidi ya uzinzi). Ikiwa unataka kugonga kichwa chako, ama ruka kutoka juu ya nyumba au fanya uzinzi. Kufuata kanuni (sheria) kunayafanya maisha yetu kuwa bora zaidi.)

II.                Elifazi Akizungumza kwa Niaba ya Shetani

A.                Soma Ayubu 4:12-14. Ni saa ngapi hapa? Elifazi yupo wapi? (Ni wakati wa usiku na Elifazi yupo kitandani.)

1.                  Je, wewe unaona kwamba usiku unatisha zaidi kuliko mchana? Kwa nini?

B.                 Soma Ayubu 4:15-17. Angalia jinsi “pepo” huyu anavyokuja, jinsi Elifazi anavyomchukulia, na maswali ya pepo. Je, huyu ni pepo mzuri au mbaya?

1.                  Utajibuje swali la “Je, binadamu atakuwa msafi au mwenye haki kuliko Mungu?” (Ukweli ni kwamba mwanadamu hawezi kuwa mwenye haki zaidi kuliko Mungu. Swali hili linajielekeza kwenye jibu sahihi. Hivyo, huyu anaweza kuwa pepo mzuri.)

C.                 Soma Ayubu 4:18-19. Sasa una mtazamo gani juu ya huyu “pepo?” (Huyu ni Shetani au mmojawapo wa malaika wake waliuoanguka kwa sababu kauli hii si ya kweli. Mungu alimtumaini Ayubu. Kauli hii inamaanisha kuwa Mungu hamwamini Ayubu na kwa hiyo Ayubu hapaswi kumtumaini Mungu. Hicho ndio kiini cha mjadala huu – je, Ayubu atamtumaini Mungu?

1.                  Kwa nini Shetani anazungumzia habari ya Mungu kuwahesabia malaika makosa? (Bado Shetani amekasirika kutokana na kutupwa kwake kutoka mbinguni (Ufunuo 12:7-9). Shetani anadhani kuwa kwa sababu yeye alitenda dhambi, basi Ayubu pia atamwangusha Mungu.)

2.                  Je, kuna mantiki yoyote kwako kwamba Shetani anaendelea kufanya kazi kwa bidii ili kumfanya Ayubu amkufuru Mungu?

a.                   Je, kitendo hicho kinakufundisha juu ya mateso maishani mwako?

D.                Soma Ayubu 4:20-21. Shetani anaashiria kuwa mwisho wa Ayubu ni upi? (Atakufa bila kuwa na hekima, ikimaanisha kuwa atakufa bila kuelewa sababu ya Mungu kumpondaponda.)

1.                  Ushauri wako kwa watesekao unaakisi hoja za Shetani kwa kiwango gani?

2.                  Hebu tujadili wazo hili kwa kina zaidi. Baadhi ya yaliyosemwa na Elifazi ni sahihi kabisa. Kauli sahihi kiteolojia zinawezaje kuakisi hoja za Shetani? (Ni pale zisipohusika kwenye kweli za hali halisi. Kanuni ya jumla, ambayo ni sahihi kiteolojia, ni kwamba mambo mabaya yanatokana na tabia mbaya. Hata hivyo, tunajua kwamba Ayubu hakuwa na tabia mbaya. Hivyo, hii kauli sahihi ilikuwa tu inasaidia juhudi za Shetani ili kumfanya Ayubu amkatae [amkane] Mungu.)

III.             Nadharia ya Nidhamu (Adhabu)

A.                Soma Waebrania 12:10-11. Hii inatufundisha nini kuhusu matatizo yanayoibuka maishani mwetu? (Yanaweza kuwa ni adhabu kutoka kwa Mungu ili kutufanya kuwa wenye haki zaidi.)

B.                 Soma Ayubu 5:17-18 na Ayubu 5:27. Huu ni mwendelezo wa ushauri wa Elifazi kwa Ayubu. Je, ungeuchukuliaje ushauri huu endapo ungekuwa Ayubu? (Huu ni mwendelezo wa hoja kwamba Ayubu ametenda jambo baya na kwamba anaadhibiwa. Hivyo, endapo ningekuwa Ayubu, ningekasirika.)

1.                  Je, Ayubu anapaswa kutafakari kama ametenda jambo linaloweza kumsababishia kupewa adhabu? (Ndiyo.)

C.                 Soma Isaya 64:6. Ikiwa Isaya yuko sahihi kwamba kila mtu ni mdhambi, je, Ayubu alipaswa kuichukulia nadharia ya adhabu kwa makini zaidi?

1.                  Ikiwa wewe ni mzazi, je, ulijaribu kuhakikisha kuwa wakati ulipowaadhibu watoto wako walielewa sababu ya kuadhibiwa kwao?

a.                   Ikiwa jibu lako ni “ndiyo,” je, unatarajia vivyo hivyo kutoka kwa Mungu?

b.                  Ikiwa kwa mara nyingine tena jibu lako ni “ndiyo,” je, hiyo inatufundisha nini kuhusu mateso na adhabu? (Kuna uhusiano wa moja kwa moja. Hutakuwa na haja ya kuwa na wasiwasi kuhusu sababu ya mateso. Sababu itakuwa dhahiri ikiwa utafungua macho yako. Ayubu hakuwa na uhusiano huo.)

D.                Soma 1 Wakorintho 4:4-5. Elifazi alipaswa kutumiaje ushauri huu katika kumshauri Ayubu? (Elifazi hakufahamu jambo lolote ambalo Ayubu alilikosea. Hakupaswa “kumhukumu” Ayubu kutokana na nadharia yake ya nidhamu (adhabu) pekee.)

IV.             Uadilifu Dhidi ya Kanuni za Asili (za Kiutendaji)

A.                Tuchukulie kwamba mtu ana uzito mkubwa kupita kiasi, anafanya mazoezi kidogo sana, anaugua ugonjwa wa kisukari, anachukua hatua ndogo sana kudhibiti chakula anachokula, na matokeo yake anapata matatizo ya neva, moyo au matatizo ya macho. Je, hii ni hukumu kutoka kwa Mungu?

1.                  Soma Mathayo 15:16-18 na 1 Wakorintho 6:12-13. Je, kula kupita kiasi na kutofanya mazoezi ni dhambi? (Sidhani. Ulaji kupita kiasi ni ujinga tu, na unaongozwa na kanuni za kiulimwengu. Ni sawa na kutovaa mkanda kwenye gari. Ikiwa utapata ajali, na hukuvaa mkanda, kanuni za Mungu za fizikia hazitakuonea huruma.)

B.                 Je, kuna aina mbili za nidhamu (adhabu)? Aina ya “moja kwa moja” inayotokana na ukiukwaji wetu wa kanuni za ulimwengu za kiutendaji au za uadilifu, na aina ya kanuni “zilizoelekezwa na Mungu” zilizopo katika Waebrania 12:10? (Sina uhakika Mungu anashughulika kwa kiasi gani na adhabu (nidhamu) ya “moja kwa moja.” Baadhi ya adhabu za “moja kwa moja” zinaadabisha anguko la uadilifu na adhabu nyingine za moja kwa moja zinaadabisha fikra za kibwege au uzembe. Zote mbili ni matumizi tu ya kanuni za kiulimwengu. Hata hivyo, ukweli kwamba Mungu ana kanuni (kama vile nguvu za mvutano) haimaanishi kwamba hiyo ni kanuni ya uadilifu.


C.                 Rafiki, natumaini umehitimisha kwamba mateso yanaweza kutokana na sababu mbalimbali. Unapoyaangalia mateso yako mwenyewe, au yale ya watu wengine, je, utamwomba Mungu akusaidie kuelewa sababu za kweli za mateso hayo au akupatie tu uwezo wa kumtumaini? Je, utakuwa makini zaidi kwenye tatizo la kupeleka ujumbe wa Kishetani kwa wale wanaoteseka?

V.                Juma lijalo: Juma lijalo: Adhabu ya Kupatiliza.

No comments:

Post a Comment