MPWAPWA DODOMA: MWENYEKITI WA ECT PR. JOSEPH MNGWABI AONGOZA MTAA WA MPWAPWA KATIKA UPANGAJI WA MAKUNDI YA MLIMANI NA MLUNGA KUWA MAKANISA

Mwenyekiti wa Konferensi ya Mashariki Kati mwa Tanzania Mchungaji Joseph Mngwabi.
 Waumini wa Kanisa la Waadventista Wasabato Mtaa w a Mpwapwa wamekumbushwa agizo la Yesu Kristo la kuongeza kasi ya kufanya uinjilisti katika makanisa yao ili injili iweze kuwafikia watu wengi.
Agizo hilo limetolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa Konferensi ya Mashariki Kati mwa Tanzania Mchungaji Joseph Mngwabi wakati akihutubia waumini na watu mbalimbali waliohudhuria sherehe za uzinduzi wa makanisa mawili ya Mlunga ambalo awali lilikuwa kundi la Mlunga na kanisa la Mlimani ambalo awali lilikuwa kundi la Igovu.
Mchungaji Joseph Mngwabi alisema lengo kuu la kutenga makundi hayo mawili kuwa makanisa ni kwa ajili ya kukuza kazi ya uinjilisti na kazi ya uinjilisti ni wajibu wa kila mshiriki; “Mmekomaa kiroho na ndio maana mmetengwa kuwa kanisa, nendeni mkahubiri injili” alisema mchungaji Mgwabi.
Aidha, katika hotuba zake mchungaji Mngwambi mambo mengine aliyosisitiza ni pamoja na waumini kuzingatia mafundisho sita pamoja na imani za misingi 28 ya Kanisa la Waadventista Wasabato.
Akizungumzia juu ya kutengwa kwa kanisa la Mlunga mwinjilisti Isaya Gailanga alisema kanisa la Mlunga lilianza kama tawi la shule ya Sabato mwaka 1998 ambapo yeye alikuwa na duka dogo ambalo alikuwa akifunga siku ya Jumamosi na nje aliandika “Ikumbuke siku ya sabato uitakase siku sita fanya kazi lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana Mungu wako duka hili linafungwa siku ya saba”.
Mwinjilisti Gailanga alisema watu waliguswa na kutaka kujifunza juu ya Sabato na kuanzia hapo walianzisha tawi la shule ya Sabato lililopelekea kundi na sasa Kanisa. “Nina furaha ya pekee na shukrani kwa Mungu kutuwezesha kufika hapa tulipo”, alisema Gailanga.
Sherehe hizo za uzinduzi wa kanisa la Mlimali zilihudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa taasisi za Serikali ikiwamo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa pamoja na jeshi la Magereza.
Akizungumza na Parapanda Adventist Media Center Afisa wa TAKUKURU wilaya ya Mpwapwa Bi. Nerry Mwakyusa aliwaambia waumini wa kanisa la Waadventista wasabato na Watanzania kwa ujumla kuwa rushwa ni adui mkubwa wa maendeleo hivyo waumini wanapaswa kuwa mstari wa mbele kupambana na huyo adui kwa kutoshiriki vitendo vya rushwa na kuwa majasiri kuwafichua wale wote wanaoshiriki vitendo vya rushwa.
Bi. Mwakyusa amesema pamoja na kuwa Rushwa ni kosa la Jinai kwa mujibu wa sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11 ya mwaka 2007 lakini pia kwa wakristo rushwa ni dhambi kwa mwenyezi Mungu kwa mujibu wa maandiko matakatifu Biblia.
Aidha Bi. Mwakyusa ametoa wito kwa waumini wa kanisa jipya la Mlimani pamoja na wahubiri wa injili kuikemea dhambi ya rushwa wazi wazi kwa kuwa rushwa ni kinyume na sheria za nchi na kanuni za kiimani.
Kwa upande mwingine, akitoa salamu za Mkuu wa Gereza Mpwapwa afisa Magereza Joseph Sabayo aliwaeleza waumini wa kanisa la Waadventista wasabato kuwa wengi huchukulia Magereza kama sehemu ambapo watu hufanyiwa ukatili na mateso jambo ambao si kweli. Magereza ni sehemu ya urekebishaji wa tabia za watu na mahali pa kujifunza.
Bwana Sabayo amesema, wapo watu walifika gerezani wakiwa hawajui kusoma na kuandika wakatoka gerezani wakiwa wanajua kusoma na kuandika na wapo waliotoka gerezani wakiwa na elimu ya kilimo na wengine hata degree za sheria na ujuzi mwingine.
Mkurugenzi wa mawasiliano na mahusiano ya umma jimbo la Mashariki Kati mwa Tanzania Mchungaji William Izungo aliwaomba waumini wa kanisa la Waadventista Wasabato Mpwapwa kuendeleza moyo wa kutoa huduma kwa jamii na kuanza taratibu za kuomba kibali katika gereza la mpwapwa ilikwamba wafungwa katika gereza hilo wapate fursa ya kutazama runinga ya morning star ambayo itasaidia kurekebisha tabia za watu kwani runinga hubadilisha maisha.
Kanisa jipya la Mlunga liko kilometa 76 kutoka Mpwapwa mjini na lina washiriki wapatao 26 na shughuli zao za kiuchumi ni kilimo pamoja na ufugaji; Aidha, kanisa jipya la Mlimani liko kilometa 6 kutoka Mpwapwa mjini ambalo lina washiriki wapatao 39 na shighuli za kiuchumi ni kazi za maofisini, kilimo na biashara.
Imeandaliwa na
Pr William lzungo,
Communication Director ,
East Central Tanzania Conference;
http://ectadventist.org/
Nakuletwa kwako na mwanahabari wako Pr. Haruni Kikiwa Mchungaji wa Mtaa wa Mbalizi.

No comments:

Post a Comment