UPENDO WA MUNGU KWA MWENYE DHAMBI.

WARUMI 5:7,8 "Kwa kuwa ni shida mtu kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki; lakini yawezekana mtu kuthubutu kufa kwa ajili ya mtu aliye mwema. Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye Mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu tulipokuwa tungali wenye dhambi"
Mungu amedhihirisha upendo wake kwa njia tele kupitia kazi zake za uumbaji na utunzaji.Lakini udhihirisho mkuu wa upendo wake ni ule aliouonyesha kwa wadhambi waliokuwa wamemwasi.

Wadhambi wanahitaji upendo,lakini hawastaili wanachostahili ni mauti. Lakini habari njema ni kwamba Mungu amekusudia kumkomboa binadamu kutoka mautini. Neno linasema "Mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama (zawadi) ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu, Bwana wetu" Warumi 6:23
Ni upendo wa Mungu tu ungeweza kusukuma nia hiyo. Haki ilidai wadhambi wafe, Lakini upendo wa Mungu ulitupatia mbadali- uzima wa milele.

Mungu hupenda sio tu watu wema, bali hata watu wabaya; siyo tu kwamba hupenda mtu mmoja mmoja bali watu wote. Kwa maana Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele" Yohana 3:16
Mungu hupenda hata wasio mpenda.Anawapenda watu wanaoukataa upendo wake na kupuuza neema yake, wenye kupenda dhambi kuliko kupenda haki,wachaguao njia ya mauti badala ya njia ya uzima. Mungu hupenda watu wanaomdharau na kumkataa Mwanaye ambaye alikuja kuwaokoa.

Hakuna jambo lolote linaloweza kukwamisha Mungu asifikishe upendo wake kwetu " Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu"
Hakuna kikwazo kiwezacho kukwamisha utendaji wa neema ya Mungu yenye kuokoa. Na ilihitajika upendo huo ili kutuokoa. Hakuna kitu pungufu ambacho kingeweza kufanikisha jambo hili. Kama Mungu asingekubali kumtoa Mwanaye kwa ajili ya wadhambi kamwe wasingaliokolewa. Kama Yesu asingaliacha kiti chake cha enzi na uzima wake kwa ajili ya wadhambi basi watu wangeangamia katika uovu wao milele.

Wapendwa tunamshukuru Mungu maana ni kwa sababu tu ya wingi wa Upendo wake leo tunapata wokovu. "Ninyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu.Lakini Mungu kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu,alituhuisha pamoja na Kristo yaani mmeokolewa kwa neema" WAEFESO 2:1,4,5
Huyu ndiye Mungu anayetuita kwa upendo wa pakee akisema "Njoni kwangu ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha" MATHAYO 11:28
Karibu Mungu mwenye upendo kwa wadhambi anakuita hata kama unajiona kwamba huwezi kusamehewa Njoo anakuita naye atakusaidia. "Haya njoni tusemezane asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana(kubuu), zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu. Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga maana kinywa cha Bwana kimenena haya" ISAYA 1:18-20

No comments:

Post a Comment