Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu
(2 Mambo ya Nyakati 33-35,
2 Wafalme 23)
Somo hili limetafsiriwa
kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko
yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978,
1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu
kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa
Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi
(kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu
nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya
kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza
kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com
kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org
kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa,
Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Sulemani anasema
kuwa watu wenye busara, kama ilivyo kwa watu wapumbavu na wajinga, wote
wanakufa na kuwaachia watu wengine mali zao. Zaburi 49:10. Maishani tuko na
watu wa aina mbalimbali wanaosababisha mambo tofauti tofauti kututokea. Yosia alikuwa
mtu wa Mungu, lakini maisha yake machanga yalikuwa na msukosuko, na aliuawa
vitani katika umri mdogo. Mambo haya yanaleta mantiki yoyote? Hebu tuchimbue
somo letu la Biblia ili tuone kile tunachoweza kujifunza!
I.
Asili ya Familia (Jamii)
A.
Soma 2 Mambo ya Nyakati 33:1-3. Utagundua kwamba Manase
alikuwa na umri wa miaka 12 alipoanza kutawala (alipotawazwa kuwa mfalme). Je,
umri huo unatosha kufanya maamuzi sahihi kwa Mungu? (Alitawala kwa muda wa
miaka 55. Kuna wakati aliwajibika kwa haya maamuzi ya kutisha.)
1.
Manase alikuwa na baba wa namna gani? (Baba yake
alikuwa Hezekia, mmojawapo wa mashujaa wa Mungu.)
1.
Unadhani kwa nini Manase aliugeukia uovu?
A.
Soma 2 Mambo ya Nyakati 33:9-11. Matokeo ya Manase
kuuendeleza uovu ni yapi? (Jeshi la Ashuru lilimchukua mateka na
kumdhalilisha.)
A.
Soma 2 Mambo ya Nyakati 33:12-13 na 2 Mambo ya Nyakati
33:15-17. Ikiwa tumeiacha njia ya Mungu, je, tunapaswa kuwa na wasiwasi juu ya
kilichomtokea Manase?
1.
Au, je, tuseme kwamba endapo mwisho utaishia kuwa mzuri,
basi tutataka kupitia chochote kile ambacho Mungu anakiruhusu?
1.
Je, “minyororo” na “pingu” (2 Mambo ya Nyakati 33:11)
ni mfano wa “upendo mzito?”
A.
Soma 2 Mambo ya Nyakati 33:21-24. Je, uovu huu umeviruka
vizazi kadhaa? Tunaye Hezekia ambaye ni mfalme mzuri, Manase ambaye ni mfalme
mbaya ambaye anabadilika na kuwa mzuri, na kisha mwovu Amoni kama mfalme.
1.
Ikiwa wafalme wabaya wanaweza kuwa na wana wema na
wafalme wazuri wanaweza kuwa na wana waovu, je, jambo hilo linaeleza nini kuhusu
mipaka ya malezi?
1.
Soma Kutoka 20:5-6. Mafungu haya yanaashiria nini
kuhusu wema na uovu kutoka kizazi hata kizazi? (Naamini kuwa malezi yanaleta
tofauti kubwa. Wazazi wanaweza kuwabariki au kuwadhuru watoto wao kutokana na
matendo yao. Hata hivyo, 2 Mambo ya Nyakati 33 inatuambia kuwa kuna ushuhuda wa
pekee usioendana na nadharia hiyo.)
A.
Soma 2 Mambo ya Nyakati 34:1-2. Walitunza vitabu vya
historia - 2 Mambo ya Nyakati ni kitabu cha historia. Ikiwa Yosia alisomewa historia
ya wafalme, je, anatakiwa kuhitimisha nini? (Kuna uhusiano kati ya kumtii Mungu
na maisha bora.)
1.
Vipi kuhusu asili ya familia yako? Je, unaweza kuona
jambo lile lile ambalo Yosia aliliona?
I.
Yosia
A.
Soma tena 2 Mambo ya Nyakati 33:24-25. Endapo ungekuwa
Yosia, je, ungetumia muda wako kusoma historia, au ungejihusisha zaidi kuhusu
mambo yaliyokuwa yanaendelea katika kipindi cha maisha yako? (Baba yake
aliuawa, na kisha watu wakawaua wauaji na kumweka Yosia madarakani! Hizi zilikuwa
nyakati za machafuko.)
1.
Ukipitia mafungu tuliyoyasoma, utaona kwamba katika
kipindi kirefu cha maisha ya Yosia mfalme mzuri alikuwa akitawala. Manase alimfuata
Mungu katika nyakati za mwisho za uhai wake. Sehemu hii ya mwisho ni miaka sita
ya kwanza ya maisha ya Yosia. Babaye Yosia ambaye alikuwa mwovu alitawala kuanzia
kipindi ambacho Yosia alikuwa na umri wa miaka sita hadi minane. Je, Yosia bado
ni mdogo sana kiasi cha kutotambua kwamba nyakati za machafuko ziliendana na
babaye mwovu kuwa mfalme?
A.
Soma 2 Mambo ya Nyakati 34:3. Kama unadhani kuwa
palikuwepo na athari, je, machafuko hayo yalikuwa na athari gani kwa Yosia?
(Mara kwa mara watu humrudia Mungu katika nyakati za taabu. Fungu linatuambia
(kwa kutumia hesabu ndogo) kwamba Yosia alikuwa na umri wa miaka 16 wakati
alipomtafuta Mungu.)
A.
Katika somo lililopita katika mfulilizo wa masomo haya
tulijifunza matukio yaliyotokea katika 2 Mambo ya Nyakati 34:4-15. Kwa ufupi,
Yosia alivunjavunja, kuzisagasaga, na kuchoma kila kitu kilichohusiana na ibada
ya sanamu. Kisha alikarabati na kujenga hekalu la Mungu. Katika kipindi hicho
cha ukarabati, kitabu cha torati kilipatikana. Hebu tusome 2 Mambo ya Nyakati
34:18-19. Kwa nini Yosia aliyararua mavazi yake aliposikia neno la Mungu
likisomwa mbele yake kwa mara ya kwanza kabisa? (Soma 2 Mambo ya Nyakati
34:20-22. Yosia alitambua kuwa watu walikuwa wanakiuka maelekezo ya Mungu. Kutokana
na kutokutii huku, Yosia aliujali sana (aliogopa) mtazamo wa Mungu kwa watu.)
A.
Soma 2 Mambo ya Nyakati 34:23-25. Hulda nabii mke ana
ujumbe maalum kwa Yosia – kwamba maafa yanakuja kwa sababu watu hawakumfuata
Mungu.)
1.
Endapo ungekuwa Yosia, je, mambo gani yangekuwa
yanaendelea kukupitia mawazoni mwako? (Kimsingi, hiki ndicho alichokuwa
anakiogopa. Yumkini mwitiko wake ni kwamba, “Hili si kosa langu! Sikuwa ninafahamu.
Mimi ni mtu mwema.”
A.
Soma 2 Mambo ya Nyakati 34:26-28. Mungu anao ujumbe
mwingine kwa Yosia. Angalia anachokibainisha Mungu kuhusu Yosia na kile
asichokibainisha. Mungu aliacha jambo gani? Unadhani kwa nini Mungu aliliacha?
(Mungu anaubainisha mtazamo wa Yosia, Mungu habainishi kazi yote ambayo Yosia
amekuwa akiifanya katika kuangamiza sanamu na kulijenga upya hekalu.)
1.
Kuna lipi la sisi kujifunza katika zama za sasa? (Mungu
anajali sana mitazamo yetu.)
A.
Soma 2 Mambo ya Nyakati 34:29-33. Ikiwa Yosia aliahidiwa
kuwa hatashuhudia maafa, kwa nini alifanya hivi? (Kwa sababu ya mtazamo wake. Alitaka
kuyaendeleza mapenzi ya Mungu pamoja na watu. Hakuwepo tu kwa ajili ya kuyaokoa
maisha yake mwenyewe.)
A.
Soma 2 Wafalme 23:29-30. Tulijadili mada hii pia katika
somo la awali. Shujaa mkuu wa Mungu, Yosia, anauawa na Farao-neko katika vita visivyokuwa
na umuhimu. Je, unawafahamu watu wema waliokufa mapema sana kabla ya muda?
1.
Unadhani kwa nini Yosia alifariki katika hivi vita? Kwa
nini Mungu hakumlinda? (Nadhani hii inakwenda nyuma zaidi kwenye ahadi
aliyopewa katika 2 Mambo ya Nyakati 34:26-28, kwamba Mungu hatamruhusu ayaone
maafa yaliyokuwa yanaijia nchi yake.)
a.
Hebu tutafakari jambo hili kidogo. Yosia alikuwa mtu
mwema maishani mwake mwote. Lilikuwa kosa la nani kwamba maisha yake
yalikatishwa akiwa bado mdogo? (Ilikuwa ni kosa la watu waovu waliotangulia
mbele yake.)
a.
Hiyo inatufundisha nini kuhusu watu wema kuteseka na
kufariki? (Mara nyingi matatizo yetu huwa tunajisababishia wenyewe. Lakini,
Yosia alifariki kwa sababu ya dhambi za watu wengine. Hili ndilo tatizo la
kuishi kwenye ulimwengu uliojaa uovu.)
a.
Vipi kuhusu wajibu wa Mungu katika jambo hili? Je,
Mungu angeweza kumwacha Yosia aishi maisha marefu na yenye mafanikio, na kisha kurejea
katika wakati muafaka katita tarehe ya uangamivu wa taifa? (Huu ndipo wakati
ambao mara kwa mara wanadamu wanaurejea, tunatilia shaka na kujenga hoja kwamba
kwa nini Mungu hakutenda mambo kwa njia nyingine tofauti. Tunatakiwa tu
kutumaini na kuyaamini maamuzi ya Mungu.)
1.
Hebu tuangalie jambo hili kwa mtazamo mwingine. Soma 2 Mambo
ya Nyakati 35:20-22. Je, hii inaashiria dosari ya aina fulani kwa Yosia kwa
kifo chake? (Ndiyo. Tunaweza kuelewa kwa nini Yosia hakuweza kufikiria kuwa
Farao-neko alikuwa mjumbe wa Mungu. Lakini Neko alikuwa na ujumbe kutoka kwa
Mungu kama inavyooneshwa kwenye matukio yaliyofuatia. Nadhani hitimisho ni
kwamba kuna mambo mengi sana katika matukio yanayotutokea maishani. Uamuzi wetu
mkubwa ni kuwa na mtazamo wa kumtumaini Mungu na kulitii neno lake.)
I.
Maelezo ya Hezekia
A.
Soma 2 Wafalme 20:1-3. Utakumbuka kwamba tulipochunguza
asili ya familia ya Yosia, Hezekia alikuwa babu wa babu yake na alikuwa mtu
mwema. Hezekia ana hoja gani, kwamba maisha yake yasikome? (Kwamba yeye ni mtu
mwema. Hiki ndicho haswaa ambacho tumekuwa tukikijadili kwamba ni jambo la
kufikirika, watu wema wanapaswa kuwa na maisha mema.)
A.
Soma 2 Wafalme 20:4-6. Je, umetiwa moyo? Unamwambia Mungu
kwamba ulikuwa na umeendelea kuwa mtu mwema, na Mungu anayaongeza maisha yako
na kuilinda kazi yako na nchi yako katika kipindi chote cha maisha yako? (Hivyo
ndivyo haswaa tunavyotamani mambo yawe tunapomtumaini Mungu.)
A.
Soma 2 Wafalme 20:12-13. Je, unapenda kuwaonyesha watu
vitu vizuri ulivyonavyo? Je, unaonyesha mali zako nzuri ulizonazo kwa wageni?
A.
Soma 2 Wafalme 20:14. Mfalme Hezekia haonekani
kutatizwa anapowaonesha mawakala wa Mfalme wa Babeli dhahabu yake. Kwa nini?
(Babeli ilikuwa nchi ya mbali, na Mungu aliahidi kumlinda (2 Wafalme 20:6).)
A.
Soma 2 Wafalme 20:15-18. Kama tunavyofahamu kutokana na
kujifunza habari za Yeremia, Babeli ni tishio la karibu. Hatimaye Babeli
iliiangamiza Yerusalemu pamoja na hekalu. Angalia tena mpango halisi wa Mungu
kwa ajili ya kifo cha Hezekia, na jinsi kuongeza muda wa kuishi wa Hezekia kulivyobadili
historia. Je, tunapaswa kufikia hitimisho gani?
A.
Rafiki, sote tunadhani kwamba maisha yetu ni ya muhimu
sana – na kimsingi ni ya muhimu kwetu. Lakini, katika mpango mzima wa maisha
sisi si wa muhimu kiasi hicho. Linapokuja suala la mkono wa Mungu kwa ajili ya
mstakabali wetu tunatakiwa kumtumaini. Je, utafanya uamuzi wa kuyatumaini
mapenzi ya Mungu sasa hivi kwa ajili ya maisha yako?
I. Juma lijalo: Nira ya Yeremia.
No comments:
Post a Comment