NENO LA LEO - MAREHEMU ANAYETEMBEA

Ufunuo 3:1 "..Nayajua matendo yako, ya kuwa una jina la kuwa HAI, nawe UMEKUFA".
��Kuna kisa cha kusikitisha cha binti mmoja aliyekuwa anashikiliwa na polisi akisaidia upelelezi wa tukio la mwenzie aliyemsindikiza kutoa mimba, kufia kwenye chumba cha daktari baada ya kupoteza damu nyingi. Daktari alitoloka na binti akabaki mikononi mwa polisi akidaiwa kuhusika na mauaji hayo. Jambo la kusikitisha zaidi mabinti wote walikuwa waimbaji wa kwaya ya kanisa fulani, aliyefariki aliambukizwa uja uzito na mwalimu wa kwaya, ambaye alikataa kuwa hajahusika.
��Neno la leo linasema kuna watu wanaoonekana kuwa wako hai kumbe wamekufa. Sifa moja kubwa ya mtu aliyekufa ni ufahamu kupotea, yaani milango mitano ya fahamu inakuwa haifanyi kazi. Mishipa ya fahamu ya marehemu yenye kazi ya Kusikia, Kuona, Kuonja, Kunusa na Kugusa, inakuwa imekufa. Ndivyo ilivyo kwa Mkristo au Mtu yeyote anayejiita mtu wa Mungu, huku anafurahia kufanya dhambi, mtu huyo ni Marehemu, hana fahamu, anaweza kuimba usizini tena kwa msisitizo, hata kwa kupandisha sauti juuuu, wakati yeye mwenyewe ni mkora wa mapenzi. soma - Waefeso 2:1-2.
��Mtu anaweza kuomba "Utusamehe dhambi zetu kama nasi tunavyowasamehe waliotukosea", baada ya Ibada utasikia akisema "mtu fulani amenitoka sitaki hata kumuona", kuna watu hawapendi kutokana na kasoro zao au basi wivu tu. Marehemu kiroho, anaweza kuimba wimbo wa kukemea dhambi, akimaliza utashangaa, hasira juu, ugomvi, masengenyo, uongo, wivu, husuda, mahaba na kila uchafu unaotendwa kwa siri. Ukiwaona watu wanajaa kwenye majumba ya Ibada, wakiimba mapambio ya kuabudu na kusifu, unaweza kudhani ni wacha Mungu, kumbe ni marehemu, hawakomi kutenda dhambi.
��Laana, vilio, majuto, kukosa amani na matumaini, mikosi na dhoruba mbalimbali zinazoikumba jamii yetu ni kutokana na Marehemu wanaotembea kuzidi kuongezeka katika majumba ya Ibada. Dhambi zinakata 'Network' kati yetu na Mungu, marehemu akiomba Mungu anacheka wala hasikii (Mithali 1:22-31), japo shetani anaweza kujibu maombi wakifikiri ni Mungu, na wakaendelea hadi kufia dhambini na kupotea milele.
��Haya vijana kwa wazee! Wakati umewadia tena wa kuunganishwa na Mungu, yatosha kuishi maisha yaliyo chini ya viwango vya mbinguni, na kuendelea kuwa chini ya mamlaka ya adui kwa hila. Mlango wa rehema ungali wazi, ni fulsa ya kila mmoja kuokolewa na kupewa ushindi daima.
BWANA AWAANGAZIE NURU YA USO WAKE NA KUWAPA AMANI. NAWATAKIA SIKU NJEMA.
Na: Ev Eliezer Mwangosi - Tel. 0767210299. Email. eliezer.mwangosi@yahoo.com

No comments:

Post a Comment