LESONI | SOMO LA 11 | SABATO|

Somo limetafsiriwa na Mgune Masatu

(Mwanzo 2, Marko 2, Yohana 1, Mathayo 12)
Somo hili limetafsiriwa kutoka katika Copr. 2011, Bruce N. Cameron, J.D. Marejeo yote ya maandiko yametoka kwenye tafsiri ya New International Version (NIV), copr. 1973, 1978, 1984 International Bible Society, isipokuwa kama itaelezwa vinginevyo. Nukuu kutoka kwenye tafsiri ya Biblia ya NIV inatumika kwa ruhusa ya Wachapishaji wa Biblia wa Zondervan. Majibu yaliyopendekezwa yanapatikana kwenye parandesi (kwenye mabano). Somo limekaa kimtazamo kwamba mwalimu anatumia ubao au sehemu nyingine yoyote ambayo inaweza kuonekana na wanafunzi. Kama huwa una kawaida ya kupokea somo hili kwa njia ya barua pepe na hukulipata kwa juma moja, unaweza kulipata kwa kubofya kwenye www.lesoni.blogspot.com kwa lugha ya Kiswahili na http://www.GoBible.org kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha nyingine kama vile Kifaransa, Kijerumani. Omba kwa ajili ya uongozi wa Roho Mtakatifu unapojifunza.
Utangulizi: Ninaipenda Sabato! Kwa ujumla, ni vigumu sana kwangu kupata muda wa kupumzika. Niwapo nyumbani, na kuona jambo linalotakiwa kufanyika, karibia mara zote huwa ninalifanya. Niwapo kazini, mara zote huwa nina jambo ambalo lazima nilifanye. Muda mwingine wowote ule tofauti na muda wa Sabato, huwa ninajisikia hatia (au jambo linalofanana au kukaribiana na hilo) ninapopumzika wakati kuna mambo yanayotakiwa kutekelezwa. Hata hivyo, katika siku ya Sabato, hatia yangu huwa inatoweka. Nianzapo kufikiria juu ya kazi ninayotakiwa kuifanya, huwa ninajisemea, “Hii ni Sabato, kazi haina nafasi.” Huu ni mbaraka mkubwa kiasi gani kuwa na muda wa kupumzika pasipokuwa na hatia! Sabato ni fundisho muhimu la Biblia, hivyo hebu tuzame mara moja kwenye somo letu!
I.                   Jinsi Ilivyoanza
A.                Soma Mwanzo 1:31 na Mwanzo 2:1. Je, ilimchukua Mungu muda gani kuumba ulimwengu? (Siku sita.)
1.                  Unadhani angeweza kuumba kwa muda mfupi zaidi? (Soma Mwanzo 1:14-19. Tunaona kwamba Mungu aliumba jua, mwezi na nyota, na kuzifanya zianze kufanya kazi siku moja. Niwazavyo mimi ni kwamba ikiwa aliweza kufanya hivyo kwa siku moja, hakuna kisichowezekana kwa Mungu.)
2.                  Je, Mungu angeweza kutumia muda mwingi zaidi kuumba ulimwengu? (Ndiyo, ikiwa angeamua kufanya hivyo.)
B.                 Soma Mwanzo 2:2-4. Ikiwa Mungu angeweza kutumia muda mfupi zaidi au mrefu zaidi kuumba ulimwengu, unadhani kwa nini alitumia siku sita? (Soma Marko 2:27-28. Mungu alifanya hivyo kwa ajili yetu. Alitaka tupate muda wa kupumzika.)
1.                  Angalia tena Mwanzo 2:3. Unadhani inamaanisha nini kusema kwamba Mungu “akaibarikia siku ya saba na kuitakasa?” (Kitu kilicho kitakatifu huwekwa wakfu, ni cha kipekee. Sabato ni siku maalumu.)
II.                Mamlaka ya Mungu
A.                Soma Isaya 45:11-12. Jambo gani linamtokea Mungu hapa? (Mungu anapewa changamoto. Wanadamu wanambashiri Mungu kwa mara ya pili.)
1.                  Je, Mungu ana madai gani kama msingi wa mamlaka yake kwa wanadamu? (Yeye ni Muumbaji! Nimefanya utafiti wa jambo hili na kubaini kwamba madai ya msingi ya Mungu ya kuwa na mamlaka katika sehemu zote za Biblia ni kutokana na ukweli kwamba yeye ni Muumbaji wetu.)
B.                 Soma Kutoka 20:8. Sababu ya Mungu kusema kwamba tuikumbuke siku ya Sabato na kuitakasa ni ipi? (Mungu anaihusisha Sabato na uwezo na mamlaka yake kama Muumbaji. Anasema kwamba katika muda wa siku sita aliuumba ulimwengu, na hivyo katika siku ya saba tunatakiwa kupumzika kama alivyopumzika.)

1.                  Hebu tutafakari kidogo katika muktadha wa kifalsafa. Ikiwa wewe ni Shetani, na unataka kutia changamoto mamlaka ya Mungu, je, utatumia mkakati gani? Ikiwa ungekuwa Mungu, je, ungetumia mkakati gani? (Endapo ningekuwa Shetani, ningejaribu kutia mashaka juu ya uumbaji, na ningejaribu kuufanya uumbaji usiwe wa muhimu. Endapo ningekuwa Mungu, ningefanya kama ambavyo tumesoma kwenye Amri ya Nne – ningekuwa na ukumbusho wa kila juma kwamba mimi ndiye Muumbaji.)
a.                   Je, unaiona mikakati hii ikiendelea duniani? (Ndiyo, siku sita halisi za uumbaji na Sabato ya siku ya saba zinashambuliwa vikali.)
C.                 Soma tena Kutoka 20:11. Utakumbuka kwamba Musa alipokea Amri Kumi kutoka kwa Mungu. Katika usomaji wangu nimekutana na madai kwamba “siku” zilizobainishwa katika sura ya kwanza ya kitabu cha Mwanzo hazikuwa siku kama ambavyo tunazifahamu leo. Je, “siku” zilifahamikaje katika kipindi cha Musa? (Alichokiwasilisha Mungu kwa Musa hakina mjadala. Musa pamoja na watu wake walifahamu kuwa hizi zilikuwa ni siku halisi.)
1.                  Mimi si mwanasayansi. Mimi ni mjenga hoja. Kuna watu wengi wanaojiita Wakristo, wakiwemo wa kanisani kwangu, ambao hawaamini juu ya siku sita halisi za uumbaji. Tuweke pembeni suala la sayansi. Je, hitimisho sahihi ni lipi ikiwa ulimwengu haukuumbwa kwa siku sita halisi? (Mungu alidanganya. Hakuna nafasi ya kujadili kwamba wanadamu katika kipindi cha Musa walikuwa watu wa kale sana (washamba) na wasingeweza kuelewa, kwa hiyo Mungu aliwaambia mambo yasiyo na mantiki. Mungu hakutakiwa kutoa maelezo yoyote mahsusi kuhusu Uumbaji wake. Lakini, alifanya hivyo. Katika Mwanzo 1 na Kutoka 20 amezungumza kwa umahsusi kabisa.)
a.                   Ikiwa Mungu alidanganya, je, hitimisho lenye mantiki linalofuata ni lipi? (Mungu alidanganya kuhusu jambo lile lile ambalo anadai kuwa ndio msingi wa mamlaka yake kwa wanadamu. Jambo hili linajikita kwenye kiini cha jambo linalomzungumzia Mungu. Linajikita kwenye kiini cha suala la kuwa Mkristo.)
D.                Soma Yohana 1:1-4 na Yohana 1:14. Je, “Neno” ni nani? (Yesu.)
1.                  Biblia inasema nini kumhusu Neno na uumbaji? (Inasema kwamba Yesu ndiye Muumbaji wa Mwanzo 1. Ndio maana kuyakubali maelezo ya uumbaji ni muhimu katika kuyakubali mamlaka ya Yesu.)
III.             Sabato Inatakiwa Kufananaje?
A.                Soma Mathayo 12:1-2. Je, mashtaka gani yanatolewa dhidi ya Yesu? (Hawadhibiti wanafunzi wake vizuri. Wanavunja Sabato.)
B.                 Soma Mathayo 12:3-5. Je, jibu la Yesu linafanana na jibu ambalo watoto wetu wangejibu – kwamba ndugu yangu naye pia anafanya jambo hilo hilo? Usiniadhibu, naye pia anafanya hivyo hivyo!
1.                  Je, wanafunzi wa Yesu ni sawa na makuhani wanaofanya kazi hekaluni?


C.                 Soma Mathayo 12:6-8. Hebu subiri kidogo! Yesu anasema jambo kubwa zaidi ya “kila mtu anafanya hivyo.” Je, madai ya Yesu ni yapi? (Anasema kwamba wanafunzi wake ni sawa na makuhani wanaofanya kazi hekaluni kwa sababu Yesu ndiye sababu ya kuwepo kwa hekalu. Zaidi ya hapo, Yesu anasema kuwa ana mamlaka ya kuamua kilicho sahihi kufanyika siku ya Sabato.)
1.                  Ikiwa Sabato ilikuwa inaelekea kutoweka, je, Yesu angejibu kama alivyojibu? (Hapana. Yesu hasemi chochote juu ya kwamba Sabato haitufungi tena. Badala yake, anasema kuwa yeye ndiye “Bwana wa Sabato.”)
2.                  Yesu anamaanisha nini anaposema, “Nataka rehema, wala si sadaka?” Na, kwa nini wanafunzi wake “hawana hatia?” (Angalia mwelekeo wa mifano anayoitoa Yesu. Mfano wa kwanza unaonesha rehema kwa watu wenye njaa. Wa pili unahusu kuwasaidia watu waliokuja hekaluni. Katika mambo yote mawili, kuwahurumia wanadamu ni jambo la muhimu zaidi kuliko mambo yaliyoandikwa katika sheria.)
a.                   Nakumbuka siku moja nilipokuwa kwenye bustani ya wanyama pori pamoja na kundi la kanisa. Mtu mmoja pamoja na mkewe walikuwa na watoto wadogo ambao walikuwa wanalia kwa sababu hali ya hewa ilikuwa ya joto na hivyo watoto walihitaji kinywaji cha baridi au chakula kitamu kilichogandishwa (ice cream). Wazazi hawa hawakuwanunulia watoto wao kitu chochote kwa sababu ilikuwa Sabato. Unadhani Yesu angeuchukuliaje uamuzi huo?
D.                Soma Mathayo 12:9-12. Je, unaona dosari gani kwenye mantiki ya Yesu? (Kondoo anateseka. Jambo hili linaonekana kama ni la dharura. Mtu aliyepooza mkono hana udharura.)
1.                  Kama niko sahihi katika kuonyesha huu utofauti, je, Yesu anatoa fundisho gani? (Bila kujali kama una jambo la dharura au la sio muhimu. Suala pekee ni endapo unatenda jambo jema siku ya Sabato. Ikiwa unatenda jambo jema, basi unachokifanya ni sahihi.)
2.                  Mara kwa mara huwa ninasema kuwa Biblia ni mali isiyohamishika yenye ukomo. Jambo lolote la kujifunza lililojipenyeza na kuingia kwenye Biblia lazima litakuwa la muhimu. Je, jambo la muhimu la kujifunza hapa ni lipi? (Huu ni uthibitisho thabiti kwamba utunzaji wa Sabato utaendelea. Haya ndio maelekezo ya namna ya kuitunza Sabato.)
E.                 Soma Mathayo 12:13-14. Je, viongozi wa dini wanafanya jambo gani siku ya Sabato? (Hawakuwa wakifanya jambo jema. Walikuwa wanapanga mauaji!)
F.                  Soma Mathayo 24:15-21. Yesu anazungumzia juu ya kuangamizwa kwa hekalu kulikofanyika mwaka wa 70 BK. Je, itakuwa ni ukiukaji wa Sabato kukimbia mauaji siku ya Sabato? (Kwa hakika hiyo itakuwa ni kutenda “jambo jema.”)
1.                  Endapo niko sahihi, je, Yesu anazungumzia jambo gani? (Majira ya baridi ni kipindi kibaya sana kuweza kukimbia na kutoroka. Hitaji kubwa litakuwa ni kufurahia Sabato yako, sio kukimbia katika jitihada za kuyaokoa maisha yako. Nadhani hiyo ndio mantiki ya jambo hili.)
2.                  Angalia suala la muda. Ikiwa Sabato ilikomea msalabani, je, kauli ya Yesu ingekuwa na mantiki yoyote? (Yesu alikusudia Sabato iendelee kusalia pamoja na umuhimu wake.)

G.                Soma Ufunuo 14:6-7. Huu ni ujumbe wa siku za mwisho. Je, Sabato ina wajibu gani hapa? (Utakumbuka kwamba Sabato iliumbwa kuwa kumbukumbu ya uumbaji. Wito wa kumwabudu Muumbaji unaihusisha Sabato moja kwa moja.)
H.                Rafiki, baadhi ya watu wanaosoma somo hili wanaweza kuwa na mtizamo usio sahihi juu ya utunzaji wa Sabato na wanaweza kuwa hawajauelewa ujumbe juu ya rehema. Wengine wanaweza kuwa hawajali kumbukizi ya kila juma juu ya mamlaka ya Mungu, na kupoteza muda huru uliotengwa kwa ajili ya kupumzika pasipo kujisikia hatia. Je, utafanya uamuzi leo kujaribu kuitunza Sabato kwa usahihi?

IV.             Juma lijalo: Kifo na Ufufuo.

No comments:

Post a Comment